Header Ads

Waziri Mhagama -Tafiti zinaonesha maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 80,000 mwaka 2012 hadi kufikia watu 72,000 kwa mwaka katika mwaka 2017


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amezindua taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi wa mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey) tarehe 13 Aprili, 2019 Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo alieleza kuwa utafiti huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali imeendelea kupambana na ugonjwa wa Ukimwi kwa kuonesha juhudi za kupungua kwa  kiwango cha maambukizi mapya na kupungua kwa vifo vinavyotokana na Ukimwi. 

“Tafiti zinaonesha maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 80,000 mwaka 2012 hadi kufikia watu 72,000 kwa mwaka katika mwaka 2017, vilevile takimu zinaonesha kupungua kwa vifo vinavyotokana na Ukimwi kutoka watu elfu 70 kwa mwaka katika 2010 hadi kufikia vifo elfu 32 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2017,” alieleza Mhagama

Alisema kuwa katika kuthibitisha hilo, kiwango cha maambukizi ya Ukimwi nchini kinazidi kupungua ambapo mwaka 2012 matokeo ya utafiti kama huo yalionesha kuwa kiwango cha maambukizi kilikuwa ni asilimia 5.1 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 na matokeo ya mwaka 2016 – 2017 kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7.

Waziri Mhagama alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa watu waliopima afya zao kwa hiari wanaongezeka kutoka tafiti moja hadi nyingine, kati ya watu hao wanawake waliopima ni wengi kuliko wanaume.

Sambamba na hilo, amewapongeza wanawake kwa ujasiri na moyo wa kujali afya zao, pia kuwahimiza wanaume kujitokeza kwa wingi kupima ili wafahamu hali zao za kiafya.

Hata hivyo, Waziri Mhagama ametaka kila Mkoa na Halmashauri zote nchini kujadili matokeo ya utafiti huo kwa undani katika kamati za VVU na Ukimwi kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji ili kuelewa hali ilivyo katika maeneo yao na kuandaa mipango madhubuti ya kudhibiti ongezeko la maambukizi mapya ikiwemo kuongeza upatikanaji wa huduma stahiki kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).

Get it on Google Play

No comments:

Powered by Blogger.